Dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la wasiwasi na msongo katika muongo uliopita.

Ripoti ya ‘Hali ya Afya ya Kihisia Duniani 2025’ inaonesha kuwa asilimia 39 ya watu wazima waliohojiwa duniani walikuwa na wasiwasi mkubwa siku moja kabla ya utafiti, huku asilimia 37 wakiripoti msongo wa mawazo. Utafiti huu ulifanywa na Taasisi ya Gallup katika nchi na maeneo 144, ukihusisha watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi. Ingawa viwango vya wasiwasi vilishuka kidogo mwaka 2024 na karibu na viwango vya kabla ya janga, bado wako juu kwa alama tano ikilinganishwa na mwaka 2014.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, maeneo yenye migogoro yalibainika kuwa na viwango vikubwa vya wasiwasi na msongo wa mawazo miongoni mwa wakazi wake. Aidha, asilimia ya waliolalamikia maumivu ya mwili iliongezeka kwa asilimia 2 hadi kufikia asilimia 32. Viwango vya huzuni (asilimia 26) na hasira (asilimia 22) havikubadilika sana, lakini hisia zote hasi ziko juu zaidi ikilinganishwa na mwongo mmoja uliopita. Wanawake wameripoti viwango vya juu zaidi vya huzuni, wasiwasi na maumivu ya mwili kuliko wanaume duniani.

Matokeo haya yatawasilishwa kwa umma kwenye Jukwaa la Afya Duniani litakalofanyika Berlin, likiwakutanisha maelfu ya viongozi wa kisiasa, wachumi, wafanyabiashara na viongozi wa utawala. Waandishi wa ripoti hiyo wanasisitiza ongezeko la hali ya wasiwasi na msongo kama suala linalojulikana kimataifa, lakini wakosoaji wanasema viongozi wengi huzingatia zaidi viashiria vya kiuchumi na kupuuza afya ya kihisia. Wataalamu wanaonya kwamba hisia hasi hupelekea kupungua kwa umakini na uimara wa jamii, hivyo kuifanya jamii kuwa dhaifu mbele ya changamoto.

Comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *