Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema kuwa bei za nishati katika Umoja wa Ulaya zinaendelea kuwa juu na hii inaathiri ustawi wa kaya na ushindani wa viwanda. Katika hotuba yake mbele ya Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, alieleza kuwa sababu kuu ya hali hii ni utegemezi wa Ulaya kwa mafuta ya fosili yanayoagizwa kutoka nje na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa. Pia alisisitiza kwamba miundombinu chakavu na kodi za juu zimechangia kupanda kwa gharama.
Von der Leyen alisema baadhi ya masuala yatakayopewa kipaumbele katika mkutano wa viongozi utakaoanyika Brussels ni pamoja na ushindani wa viwanda, upatikanaji wa makazi ya gharama nafuu, na nishati. Alipendekeza kwamba suluhisho liko katika kuongeza uzalishaji wa nishati mbadala ya ndani kama vile jua, upepo, umeme wa maji, jotoardhi na nyuklia. Pia aliangazia kuwa asilimia kubwa ya gharama za nishati kwa makampuni na kaya zinatokana na kodi na ushuru.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume, asilimia 34 ya gharama za nishati kwa makampuni na asilimia 42 ya bili za nishati kwa kaya ni kodi. Katika sekta ya viwanda, umeme una kodi hadi mara 15 zaidi ikilinganishwa na gesi asilia. Von der Leyen alitoa wito wa hatua za pamoja katika ngazi ya Umoja wa Ulaya na kitaifa, na akabainisha kuwa jitihada mpya za kuboresha na kuunganisha miundombinu ya umeme zitatangazwa, lakini pia akaongeza kuwa kuachana na gesi na mafuta ghafla si rahisi kwa sasa.

Toa Jibu