Uchunguzi uliofanywa na mashirika ya watumiaji barani Ulaya umebaini kwamba asilimia 70 ya bidhaa zinazouzwa kutoka kwenye majukwaa ya mtandaoni ya Shein na Temu hazizingatii kanuni za usalama za Ulaya. Utafiti huu ulijumuisha bidhaa 162 zikiwemo vinyago vya watoto wadogo, chaja za USB na mikufu, ambapo bidhaa 112 zilionyesha aina mbalimbali za kasoro za kiusalama na sheria zinakataza ziuzwe barani humo.
Katika vipimo vilivyofanyika, vinyago kutoka Shein na Temu vilionekana kuwa na tatizo la sehemu ndogo zinazoweza kujitenga na kusababisha hatari ya kukabwa, pamoja na uwepo wa kemikali hatari kama sumu na miundo isiyo salama. Kwa chaja za USB, karibu zote zilibainika kuwa na upungufu, huku zingine zikifikia joto la zaidi ya 100°C wakati wa matumizi, na ni chaja moja tu kutoka kila jukwaa iliweza kupita vipimo.
Mikufu nayo ilipimwa na baadhi zilionekana kuwa na kiwango kikubwa kupita kiasi cha metali nzito zenye madhara kiafya ikiwemo kadimiamu, ambapo katika baadhi ya sampuli, viwango vilikuwa hadi mara 8,500 zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa. Waziri wa Mazingira wa Ubelgiji ameanza kampeni mpya ya ukaguzi ili kudhibiti uingizwaji na uuzaji wa bidhaa zenye madhara, huku wateja wakishauriwa kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa kutoka majukwaa haya.









